KAMATI YA KITAIFA YA USIMAMIZI WA UANDAAJI MPANGO KAZI WA KITAIFA WA HAKI ZA BINADAMU NA BIASHARA YAKUTANA NA TIMU YA WATAALAM YA UANDAAJI WA MPANGO

KAMATI YA KITAIFA YA USIMAMIZI WA UANDAAJI MPANGO KAZI WA KITAIFA WA HAKI ZA BINADAMU NA BIASHARA YAKUTANA NA TIMU YA WATAALAM YA UANDAAJI WA MPANGO
Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Uandaaji wa Mpango kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara imekutana na Timu ya Wataalam ya Uandaaji wa Mpango kazi wa Kitaifa wa haki za binadamu na biashara, Februari 21, 2015, Jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho Timu wa Wataalam imekabidhi Rasimu ya Awali ya mpango kazi wa Kitaifa wa haki za binadamu na biashara kwa Kamati ya Usimamizi wa uandaaji wa mpango huo kwa lengo la kupitia, kuifanyia maboresho na kuidhinisha Rasimu hiyo.
Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake Dkt. Franklin J. Rwezimula ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, ilipokea Rasimu hiyo ya Awali na kuipitia pamoja na kuifanyia maboresho ikiwa ni moja ya hatua muhimu katika uandaaji wa mpango huo.
Akizungumza na Waandishi wa habari Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Mhe. Mohamed Khamis Hamad ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati hiyo amesema, mpango kazi huo unaangazia shughuli zote muhimu za kiuchumi zinazoweza kumuathiri mwanadamu.
“ Tanzania inakuwa kiuchumi, ni vipi hizi shughuli za kiuchumi zitakwenda sambamba na haki za watu, kam vile tunavyosikia kwamba kuna migogoro ya wawekezaji na wananchi wa maeneo ya karibu, kuna wengine hawapewi mikataba ya kazi, wengine hawana vifaa vya kujilinda wakati wa kazi, kuna maswala ya kimazingira, hizo zote ni shughuli za kibiashara ambazo kwa njia moja au nyingine zinaweza kumuathiri huyu mwanadamu “. Amesema Mhe. Hamad
Naye, Dkt. Noel Komba, Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati amesema Rasimu hiyo ipo katika hatua za mwisho na matarajio ni kwamba baada ya kukamilika, mpango huo utatoa fursa kwa Wawekezaji katika sekta mbalimbali na wananchi ambao ni waajiriwa pale wanapopata migogoro ya haki zao katika maeneo yao ya kazi.
Aidha, mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo la uboreshaji wa Rasimu hiyo, Kamati iliidhinisha Rasimu hiyo na sasa ipo tayari kwa hatua zinazoendelea.
Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa uandaaji wa mpango kazi wa kitaifa wa haki za binadamu na biashara ina wawakilishi kutoka Tanzania bara na Zanzibar ambapo ndani yake kuna wajumbe kutoka Serikalini, Taasisi za Serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na wataalam wa masuala ya haki za binadamu na biashara.