Majukumu ya Tume
Majukumu ya Tume
Kazi za Tume zinatekelezwa kulingana na dira, dhima na malengo ya Tume kama
zilivyoainishwa katika Ibara ya 130 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka
1977 na katika kifungu cha 6 (1) vifungu vidogo (a) mpaka (o) vya Sheria ya Tume. Majukumu
hayo ni kama ifuatavyo:
Kukuza nchini kinga na hifadhi ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii kwa mujibu
wa Katiba na Sheria za nchi;
b) Kupokea malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu kwa ujumla;
c) Kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na
ukiukwaji wa misingi ya utawala bora ;
d) Kufanya utafiti katika, kutoa na kueneza nchini elimu kwa umma kuhusu haki za
binadamu na utawala bora;
e) Inapobidi, kufungua mashauri mahakamani yanayolenga kukomesha ukiukwaji wa
haki za binadamu au kurekebisha haki zinapovunjwa au misingi ya utawala bora
inapokiukwa;
f) Kuchunguza mwenendo wa mtu yeyote au taasisi yoyote ambayo vifungu vya
sehemu hii vinahusiana navyo katika utaratibu wa kawaida wa kutekeleza kazi za
ofisi yake au utendaji wa kazi unaokiuka mamlaka yake;
g) Kupeleleza au kuchunguza malalamiko yanayohusiana na utekelezaji au utendaji wa
watu wanaoshikilia ofisi katika utumishi wa Serikali, mamlaka za umma au vyombo
vya umma, ikijumuisha taasisi binafsi na watu binafsi ambapo malalamiko hayo
yanadaiwa kuwa ni ya matumizi mabaya ya madaraka, huduma za upendeleo kwa
mtu yeyote, ikiwa ni mlalamikaji au mtu mwingine, katika kutekeleza kazi zao za
kiserikali au umma;
h) Kutembelea Magereza na mahala pengine wanamozuiliwa watu au sehemu
zinazofanana kwa madhumuni ya kutathmini na kukagua hali za watu wanaozuiliwa
sehemu hizo na kutoa mapendekezo yatakayowezesha kurekebisha kasoro zilizopo
kwa mujibu wa matakwa ya Sheria hii;
i) Kuchukua hatua za kusaidia kusahihisha, kurekebisha, kuzuia au kukomesha vitendo
vilivyotajwa katika vifungu (e), (f), (g) au (h) kutokana na njia za usawa sahihi na
haki, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kisheria;
j) Kutoa ushauri kwa Serikali na kwa vyombo vingine vya umma na taasisi za sekta
binafsi juu ya mambo maalum yanayohusiana na haki za binadamu na utawala bora;
k) Kutoa mapendekezo yanayohusiana na sheria iliyokwishatungwa au inayokusudiwa
kutungwa, kanuni, au mambo ya kiutawala ili kuhakikisha zinakubaliana na haki za
binadamu na za misingi ya utawala bora;
l) Kusaidia uridhiaji wa au utiaji saini mikataba au makubaliano yanayohusu haki za
binadamu, kuzilinganisha sheria za nchi na kufuatilia na kutathmini utekelezaji ndani
ya Jamhuri ya Muungano na Serikali na watu wengine, kwa viwango vya haki za
22
binadamu vilivyoainishwa kwenye mikataba au makubaliano au chini ya sheria za
kawaida za mahusiano ya kimataifa ambayo Jamhuri ya Muungano inawajibika nayo
m) Kwa kupitia Serikali, kushirikiana na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa
Nchi za Afrika, Jumuia ya Madola na taasisi nyingine zenye uhusiano baina yao,
miongoni mwao au ya kikanda na taasisi za nchi za nje ambazo zina uzoefu katika
ulinzi na ukuzaji wa haki za binadamu na utawala bora;
n) Kuchukua hatua zifaazo kwa ajili ya ukuzaji na uendelezaji wa upatanishi na
usuluhishi miongoni mwa taasisi na watu mbalimbali ambao hufika au hufikishwa
mbele ya Tume;
o) Kufanya kazi nyinginezo zozote kama zinavyoweza kuelezwa katika sheria nyingine.
Aidha, ibara ya 131 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeainisha maeneo
ambayo Tume haina mamlaka kuyachunguza kama ifuatavyo.
a) Jambo lolote ambalo liko mbele ya Mahakama au chombo kinginecho cha
Kimahakama.
b) Jambo lolote linalohusu uhusiano au mashirikiano kati ya Serikali ya nchi yoyote ya
nje au shirika la Kimataifa
c) Jambo linalohusu madaraka ya Rais kutoa msamaha.
d) Jambo jingine lolote lililotajwa na sheria yoyote.