Tamko la THBUB wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani 2021
Tamko la THBUB wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani 2021
NOVEMBA 23, 2021 ni kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani ambapo maadhimisho hayo mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo: “Jali maisha yako na ya wengine barabarani.”
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kama mdau katika masuala ya haki na usalama wa raia inapenda kutumia fursa hii kutoa pongezi zake za dhati kwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na vyombo vyote vinavyohusika na usimamizi wa sheria za usalama barabarani.
Aidha, Tume inazipongeza Serikali zote mbili kwa kuboresha miundo mbinu ya barabara ambayo imesaidia kupungua kwa vifo na majeruhi kutokana na ajali za barabarani.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana, bado kuna changamoto kadhaa zinazohitaji kushughulikiwa. Changamoto hizo ni pamoja na: Usimamizi hafifu wa sheria katika baadhi ya maeneo; magari ya abiria yaendayo safari ndefu kuwa na dereva mmoja; madereva wengi kutokuwa na mikataba ya ajira; ukosefu wa teknolojia bora ya ukaguzi wa magari; upotevu wa haki za waathirika wa ajali; upatikanaji wa takwimu bora; utaratibu wa utoaji wa adhabu kwa madereva, kutaja kwa uchache.
Kufuatia uwepo wa changamoto hizi Tume inashauri yafuatayo:
- 1.Serikali iendelee kuboresha miundombinu ya barabara na kusimamia sheria za barabarani kwa makini.
- 2.Serikali ihimize matumizi ya teknolojia saidizi itakayowawezesha wakaguzi kufanya kazi yao ya ukaguzi wa magari kwa ufanisi na uwazi zaidi.
- 3.Serikali iboreshe na kuongeza vituo vya ukaguzi ikiwa ni pamoja na kuwapatia Askari wa Usalama Barabarani vifaa vya kisasa ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
- 4.Kamishna wa Kazi asimamie matakwa ya sheria inayomtaka kila mwajiri kutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wake. Hii itasaidia kuweka mazingira bora ya kazi kwa madereva.
- 5.Jeshi la Polisi na wadau wengine waendelee kutoa elimu kwa madereva na wananchi kuhusu matumizi sahihi ya barabara ili kuepusha ajali.
- 6.Madereva na Wananchi waendelee kuhimizwa kuzingatia sheria za usalama barabarani.
“Jali maisha yako na ya wengine barabarani.”
Imetolewa na:
(SIGNED)
Mohamed Khamis Hamad
Makamu Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Novemba 23, 2021