ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB na LHRC watiliana saini mkataba wa nyongeza wa mashirikano

17 Aug, 2021
THBUB na LHRC watiliana saini mkataba wa nyongeza wa mashirikano

Na Said Rashid

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) zimetiliana saini mkataba wa nyongeza (Adendum) wenye lengo la kuimarisha mashirikiano katika utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu, utawala wa sheria na utawala bora.

Tukio hilo lililofanyika mara baada ya kikao cha pamoja kilichofanyika makao makuu ya Ofisi za Tume, Jijini Dodoma leo (Agosti 17, 2021) limeshuhudiwa na viongozi na maafisa kutoka LHRC na THBUB, wakiwemo Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Anna Henga na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume, Bwana Nabor Assey ambao walitia saini nyaraka hizo kwa niaba ya taasisi zao.

Viongozi wengine walioshuhudia tukio hilo kutoka THBUB ni: Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Mathew Mwaimu (Jaji mstaafu), Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Mohamed Khamis, na Wahe. Makamishna wa Tume, Dkt. Fatma Khalfan, Dkt. Thomas Masanja, na Amina Talib Ally.

Kwa upande wa LHRC ni: Mkurugenzi wa Ujengaji Uwezo na Uwajibikaji, Bi. Felista Mauya, Afisa Programu ya Uchechemuzi, Bwana Raymond Kanegene, na Mkuu wa Ofisi ya LHRC Dodoma, Bwana William Mtwazi.

Mkataba huo wa nyongeza wa mashirikiano umeainisha maeneo manne (4) makuu ya mashirikiano, ambayo ni: Uanzishaji na uwezeshaji utekelezaji wa shughuli zinazolenga kulinda na kukuza haki za makundi maalumu ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu na ubadilishanaji uzoefu na utaalamu katika michakato mbalimbali ikiwemo utayarishaji na uthibitishaji wa taarifa, uwasilishaji na usambazaji wa mapendekezo ya Universal Periodic Review (UPR) kwa umma.

Maeneo mengine ni: Ushirikiano katika shughuli za kuwajengea uwezo katika masuala ya haki za binadamu na utawala bora Viongozi wa Serikali za Mitaa, hususan Wakuu wa Wilaya na Madiwani na kuanzisha, kufuatilia na kuimarisha Klabu za haki za binadamu katika taasisi za elimu kuanzia ngazi ya Msingi hadi Chuo Kikuu.

Tume na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu zilitiliana saini mkataba wa awali wa mashirikiano katika utoaji wa elimu kwa umma na ufuatiliaji wa masuala ya haki za binadamu nchini mwaka 2018.