THBUB na MISA-TAN wasaini hati ya mashirikiano
15 Apr, 2024
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika – tawi la Tanzania (MISA-TAN) wametia saini hati ya mashirikiano ya utekelezaji wa mradi wa pamoja wa kuimarisha uelewa na utekelezaji wa haki za binadamu kupitia uandishi wa habari za kiuchunguzi.
Katibu Mtendaji wa THBUB, Bwana Patience Ntwina na Mkurugenzi Mtendaji wa MISA-TAN,Bi. Elizabeth Riziki wametia saini hati hiyo ya makubaliano leo Machi 28, 2024 katika hafla fupi iliyofanyika Makao Makuu ya Tume Kilimani jijini Dodoma na kushuhudiwa na viongozi wa juu wa pande zote mbili.
Lengo kuu la mradi huo wa miaka mitatu (2024 - 2027) ni kukuza haki za binadamu na utawala bora kwa makundi yaliyo hatarini nchini Tanzania, hususan wanawake, watoto, watu wenye ulemavu, wazee na vijana.
Kwa mujibu wa hati ya makubaliano, malengo mahususi ya mradi huo ni kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya THBUB na vyombo vya habari katika kushughulikia masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu na kukuza uwajibikaji miongoni mwa jamii.
Pia, unalenga kuongeza uelewa wa umma, hususan wanawake, watoto, vijana, wazee na watu wenye ulemavu kuhusu haki zao, kuwawezesha kupata huduma za Tume, na kufanya uchechemuzi juu ya maboresho ya sera na sheria za nchi ili kulinda haki za binadamu na haki za makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.
Vilevile, mradi huo unalenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika kuripoti masuala ya haki za binadamu na masuala mengineyo yenye maslahi kwa umma, kutaja kwa uchache.
Akiongea mara baada ya kutiwa saini kwa hati ya makubaliano ya mashirikiano, Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Mohamed Khamis Hamad ameushukuru uongozi wa MISA-TAN kwa utayari wao wa kufanya kazi na Tume na kuwa anatarajia mashirikiano hayo yatakuwa na matokeo chanya kwa taifa.
"Nina imani baada ya muda mfupi tutapata matokeo yaliyo bora na yenye maslahi kwa nchi yetu,"Mhe. Mohamed amesema.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya MISA-TAN, Wakili MsomiJames Marenga amesema kuwa mashirikiano baina ya taasisi yake na THBUByatausaidia umma kuifahamu Tume na shughuli zake na kutumia huduma zitolewazo.