THBUB YASHIRIKI MDAHALO WA WAZI KUADHIMISHA MIAKA 60 YA MUUNGANO
Katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeungana na Kituo cha AFM Radio cha jijini Dodoma kupitia kipindi cha *"Nijuze"* kufanya mdahalo kuhusu nafasi ya vijana katika kuwania nafasi za uongozi kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Mdahalo huo wa wazi uliorushwa mbashara kupitia kituo hicho umefanyika leo Aprili 26, 2024 eneo la Mnadani Kijijini Mpunguzi nje kidogo ya jiji la Dodoma.
Mgeni Rasmi katika tukio hilo alikuwa Bwana Mfungo Manyama, Afisa Vijana, akimwakilisha Mkurugenzi wa jiji la Dodoma.
Katika hotuba yake ya ufunguzi Bwana Mfungo alikipongeza Kituo cha AFM radio kwa kuandaa mdahalo huo na kuwahamasisha vijana kuwania nafasi za uongozi.
Mwakilishi wa THBUB katika tukio hilo, Afisa Uchunguzi Mwandamizi, Bwana Said Zuberi aliieleza hadhira kuwa vijana wanakabiliwa nachangamoto mbalimbali zinazopunguza ushiriki wao katika michakato ya uchaguzi hapa nchini.
Alizibainisha changamoto hizo kuwa ni pamoja na: Vijana kutojiamini; kuwa na kipato kidogo; mifumo iliyopo kutotoa fursa za kutosha; na vijana kutojihusisaha na masuala ya siasa.
Changamoto nyingine ni: Vijana kutokuwa na elimu ya kutosha; jamii kuwa na mtazamo hasi juu ya vijana; vijana kutokuwa tayari kushiriki; na vyama vya siasa kutowaamini vijana kuwa wanaweza.
Aidha, Bwana Zuberi aliwafahamisha washiriki wa mdahalo kuwa mwaka 2020 THBUB kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia iliandaa Mkakati wa kuongeza ushiriki wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika uchaguzi.
Pia, Tume inaendelea kutoa elimu ya uraia kupitia Klabu za Haki za Binadamu shuleni na vyuoni ili kuhamasisha ushiriki wa vijana katika michakato ya uchaguzi.
Aliongeza kuwa kuelekea chaguzi za 2024 na 2025 THBUB imejipanga kutoa elimu ya uraia, haki za binadamu na utawala bora kwa makundi mbalimbali ya jamii nchini.