ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

WAANDISHI WA HABARI MANYARA WAKUMBUSHWA WAJIBU WAO KULINDA HAKI ZA BINADAMU

19 Mar, 2025
WAANDISHI WA HABARI MANYARA WAKUMBUSHWA WAJIBU WAO KULINDA HAKI ZA BINADAMU

Makamu Mwenyekiti wa Tume za Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Mohamed Khamis Hamad ametoa rai kwa waandishi wa Habari wa Mkoa wa Manyara kutumia elimu ya haki za binadamu inayotolewa na Tume hiyo kuielimisha jamii na kuibua vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Rai hiyo imetolewa wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wandishi hao kuhusu masuala ya haki za binadamu yaliyotolewa katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Manyara  Machi 19,2025.

“Elimu kuhusu haki za binadamu ni nyenzo muhimu ya kuhakikisha kuwa wananchi wanazitambua na kulinda haki zao………...” amesema Mohamed.

Naye Mchunguzi Mkuu Msaidizi wa Tume ya Haki za binadamu, Bw. Halfan Botea, wakati wa uwasilishaji wa mada ya haki za Binadamu amefafanua kuwa ukiukwaji wa haki moja  huathiri haki nyingine. Hivyo, amesisitiza kuwa jamii inapaswa kuzingatia haki za binadamu ili kuwa na jamii yenye  amani na utulivu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo wameiomba Tume  kuendela kutoa  mafunzo ya mara kwa mara kuhusu masuala ya haki za binadamu kwa waandishi wa habari nchini kwa kuwa kundi hili ni wadau muhimu katika kulinda na kutetea haki za binadamu katika jamii.

Mafunzo yaliyotolewa kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara ni mwendelezo wa utoaji wa elimu ya haki za binadamu na utawala bora yanayotolewa na THBUB kwa makundi mbalimbali katika mkoa huo yakiwemo makundi ya watendaji wa kata, wanafunzi wa vyuo na shule za sekondari, wafungwa na watendaji wa magereza na vituo vya polisi. Elimu hiyo itatolewa ili kuyajengea makundi hayo uwezo wa kuzifahamu haki zao na wajibu wao katika kulinda haki za binadamu.