Wakazi wa Dodoma wanufaika Maadhimisho Miaka 20 ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Wakazi wa Jiji la Dodoma wameendelea kutembelea mabanda ya maonesho ya kupatiwa elimu pamoja na huduma zinazotolewa na wadau wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuelekea kilele cha maadhimisho ya Miaka ishirini ya Tume kinachotarajia kufanyika Septemba 15,2022.
Taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali na Binafsi zinazohusika na masuala ya Haki za Binadamu na Utawala Bora zimeshiriki maadhimisho hayo kutoka sehemu mbalimbali nchini na kupata nafasi ya kuelezea shuguhli zao kwa Wananchi waliojitokeza kutembelea maonesho hayo.
Naibu Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma,Yarerd Jamal alipotembelea maonesho hayo Septemba 13,2022 alisema kuwa amefurahishwa na maandalizi yaliyofanywa na Tume katika maadhimisho hayo na kuwataka wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi kutumia fursa nyingi zinazopatikana katika maadhimisho hayo.
‘’Nimetembelea mabanda mengi katika uwanja huu,nimefurahishwa na jinsi wananchi wanavyopatiwa huduma huduma hapa hasa katika Wakala ya Usajili ,Ufilisi na Udhamini(RITA) ambapo nimekuta foleni kubwa nawapongeza kwa jinsi mlivyojipanga natoa rai muendelee kuwahamasisha wananchi ambao bado hawajafika hapa wafanye hivyo,”alisema Mhe. Yarerd
Akiongelea wadau binafsi waliofika kuoneshs shughuli zao katika uwanja huo,alisema amejifunza mambo mengi kutoka kwao ambayo awali hakuyajua,na kuwaasa kwamba umefika wakati wa kujitokeza kupitia vyombo mbalimbali vya habari na kujitangaza ili Watanzania wawajue aidha,alitoa rai kwa Taasisi hizo hasa zile ambazo hazina Ofisi Dodoma kufanya hivyo.
“Kama mnavyojua Dodoma ni Makao Makuu ya Nchi na Serikali nzima imejikita hapa,ni vizuri Taasisi binafsi pia mkaweka Ofisi zenu hapa ili muweze kuwahudmia wananchi kutoka kila kona ya nchi kwa urahisi,nawakaribisha sana na kama mtakutana na changamoto yoyote katika kutimiza jambo hili karibuni ofisini nipo tayari ushirikiano,”aliongeza