Wanafunzi Chuo Kikuu cha Waislamu Moro watembelea THBUB, waipongeza
Wanafunzi 70 wanachama wa Klabu ya haki za binadamu Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro wakiambatana na walimu wanne (4) leo Januari 26,2024 wametembelea Makao Makuu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Kilimani jijini Dodoma na kujifunza masuala mbalimbali.
Wanafunzi hao wameipongeza Tume kwa juhudi zake za kulinda na kueneza elimu ya haki za binadamu na utawala bora nchini.
“Tumetembelea Tume na kujifunza masuala mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu ya Tume, tumefurahi sana, hakika mnafanya kazi nzuri iliyotukuka,” amesema mmoja wa wanafunzi hao.
“Nimefurahi pia kuwaona Mheshimiwa Mwenyekiti wa Tume na Makamishna wake, na jinsi tulivyopokelewa vizuri na kwa upendo mkubwa,” ameongeza.
Wakiwa katika ofisi hizo za Tume wanafunzi hao walipata fursa ya kuwasikiliza wakurugenzi na wakuu wa vitengo vilivyopo Tume wakielezea utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kupitia idara na vitengo wanavyosimamia. Vilevile, walipata nasaha kutoka kwa viongozi wa juu wa Tume.
Wanafunzi hao wametembelea THBUB kama taasisi ya kitaifa ya haki za binadamu na mlezi wa Klabu za haki za binadamu katika taasisi za elimu nchini, ili kujifunza namna Tume inavyotekeleza majukumu yake.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Klabu ya haki za binadamu Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, Bi. Asia Ashirafu kila mwaka Klabu hiyo imekuwa na utaratibu wa kutembelea taasisi mbalimbali za umma kwa lengo la kujifunza kama sehemu ya masomo yao