ZIARA YA THBUB KIWANDA CHA KAGERA SUGAR
Ujumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ukiongozwa na Mhe. Kamishna Amina Talib Ali umeendelea na ziara yake ya kukusanya maoni kutoka kwa wadau ya Uandaaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara mkoani Kagera.
Leo Septemba 25, 2024 ujumbe huo umetembelea Kiwanda cha Sukari cha Kagera kilichopo katika Wilaya ya Misenyi ambapo THBUB ilikutana na Menejimenti ya Kiwanda hicho ikiongozwa na Meneja wa Utawala na Rasilimali Watu Bw. Francis Lubangi
Katika kikao hicho Mhe. Amina alieleza kuwa lengo la ziara ya THBUB katika kiwanda hicho ni kukusanya maoni yatakayosaidia katika Uandaaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara hususani katika eneo la Haki za Watoto.
“THBUB katika kukusanya maoni imeona kuna umuhimu wa kutembelea kiwandani hiki na kuzungumza na ninyi ili tuweze kupata maoni ya pamoja katika uandaaji mpango kazi huu” amesema Mhe. Amina
Kwa upande wake Meneja wa Rasilimali Watu na Utalawa Bw. Francis Lubangi amesema kuwa kiwanda hicho kina kambi ishirini (20) ikiwemo Makazi, Nyumba za ibada, Shule za Msingi na Shule za Awali.
Bw. Lubangi aliongeza kwa kusema kuwa Kiwanda hicho kinarudisha huduma kwa jamii ambapo kimejenga Shule ya Awali na Shule ya Msingi, upatikanaji wa huduma ya afya kwa kujenga Hospitali yenye hadhi ya ngazi ya Wilaya, na Zahanati tatu (3).
“Huduma zote hizi zinatolewa bure kwa wafanyakazi na wananchi wanaoishi jirani na kiwanda hicho” amesema Bw. Lubangi