THBUB yaendelea kuchakata maoni ya mpango kazi wa haki za binadamu na biashara
ume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeendelea na Mchakato wa Uandaaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara wenye lengo la kuweka mazingira bora kwa Wafanyabiashara kuzingaita haki za binadamu wakati wakifanya biashara zao.
Hayo amesema Makamu Mwenyekiti wa THBUB Mhe. Mohamed Khamis Hamad wakati wa kifungua Kikao Kazi cha kupitia maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali, kikao hicho kilifanyika Oktoba 15, 2024 Jijini Arusha.
Mhe. Mohamed amesema kuwa THBUB kwa kushirikiana na wadau wengine imefanikiwa kukusanya maoni ya wadau kupitia vikao na mikutano ya hadhara na wananchi wanaoishi maeneo ya uwekezaji ili kupata uhalisia.
“Tumefanikiwa kupita maeneo ya Viwanda, Shughuli za uvuvi, Mahotelini na hata maeneo ya Uchimbaji wa Madini na kuzungumza na wafanyakazi na wananchi wanaozunguka maeneo hayo ”amesema Mhe. Mohamed
Aidha, Mhe. Mohamed ameongeza kwa kusema kuwa miongoni mwa changamoto zilizojitokeza katika ukusanyaji wa maoni hayo ni wafanyakazi wengi kutokua na Mikataba ya Kazi, pamoja na uwepo wa migogoro baina ya wawekezaji na jamii inayowazunguka.
“Uandaaji wa Mpango Kazi huu utasaidia kuboresha maeneo ambayo tumeona yamekua na changamoto”amesema Mhe. Mohamed
Naye ,Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dkt. Anna Henga amesema kuwa kwa miaka kadhaa kituo hicho kimekuwa kikifanya kazi ya Utetezi wa haki za binadamu katika sekta ya biashara na uchechemuzi wa Sera na Sheria kuhakikisha Mikataba na Miongozo ya Kimataifa pamoja na Sheria za nchi zinazohusiana na biashara zinatekelezwa kwa kufuata misingi ya haki za binadamu.
“Katika mchakato huu wa kutengeneza Mpango Kazi wa Biashara na Haki za Binadamu, LHRC imeshiriki kikamilifu kama sehemu ya timu ya wataalamu wa Uandaaji wa Mpango kazi huo” amesema Dkt. Anna
Kwa upande wake Bi. Joyce Deloge, Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchukua hatua ya kuandaa Mpango kazi wa haki za Binadamu na Biashara ambao utakua ni msaada mkubwa wa kusimamia masuala ya haki za binadamu katika biashara.
Pia Bi. Joyce ameeleza zaidi kuwa nchi nyingi siku hizi zimekuwa wazi ambapo upelekea wafanyabiashara kuingia nakufanya shughuli zao bila kuzingatia taratibu za nchi husika.
“Mpango kazi huu utasaidia kulinda na kukuza haki za binadamu katika sekta ya biashara nchini Tanzania “amesema Bi.Joyce
Awali Katibu Mtenda wa THBUB Bw. Patience Ntwina amesema kuwa THBUB na wadau wengine walipitia nyaraka mbalimbali ambazo ni Sera, Sheria, Mipngo na Mikakati iliyopo nchini kuhusiana na biashara na uwekezaji, kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali maoni ya wadau kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar na kuangalia uzoefu kutoka nchi nyingine ili kueza kufahamu changamoto wanazokutana nazo katika eneo hili.
Bw. Ntwina amesema kuwa kupitia Kikao Kazi hicho cha Siku Nne (4) wataalamu watatatoka na Rasimu ya Awali ya Mpango Kazi wa Kitaifa wa Biashara na Haki za Binadamu ambao utakuwa na maeneo ya vipaumbele na majukumu ya kila mdau muhimu katika uboreshaji wa haki za binadamu katika sekta ya biashara nchini.