ADEM Logo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Tunajenga utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora na utu wa mtu
ADEM Logo

THBUB yakutana na wadau Kujadili Sheria za Uhifadhi

29 Oct, 2024
THBUB yakutana na wadau  Kujadili Sheria za Uhifadhi

Serikali ina wajibu wa kutunga Sheria zinazolenga kulinda rasilimali za asili ikiwemo; misitu, wanyamapori, ardhi na vyanzo vya maji dhidi ya uharibifu unaosababishwa na shughuli za kiuchumi na kijamii zinazofanywa na  binadamu ikiwa na lengo la kuhakikisha kuwa rasilimali hizi zinatumika kwa  manufaa ya taifa nzima.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Mhe. Dkt.Thomas Masanja wakati akifungua Kikao Kazi cha Kupitia, kutoa maoni na mapendekezo kuhusu Sheria zinazohusiana na maeneo ya Hifadhi za Taifa Oktoba 28, 2024 Jijini Arusha.

Mhe. Dkt Masanja amesema kuwa Serikali pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetimiza wajibu wake wa kutunga Sheria za Hifadhi za Taifa kwa kuhakikisha kuwa maliasili, mazingira na urithi wa kiasili wa nchi unalindwa na kudumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Sheria hizi zinapaswa kuweka msingi wa uhifadhi endelevu na kusimamia matumizi bora ya rasilimali za taifa ”amesema Mhe. Dkt. Masanja.

Aidha, Mhe.Dkt. Masanja aliongeza kuwa THBUB imefanya mapitio ya Sheria mbalimbali za uhifadhi ikiwemo Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro Sura ya 284, Sheria ya Hifadhi ya Wanyama Pori Sura ya 283, Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura ya 282, na Sheria ya Misitu Sura ya 323 na kuyawasilisha serikalini.

 

“THBUB inawajibu wa kutoa mapendekezo kwa serikali na Taasisi zake kuhusu marekebisho ya Sera au Sheria zinazokinzana na haki za binadamu, ili kuhakikisha kuwa sheria hizi za nchi zinaendana na Mikataba ya Kimataifa na akikanda ya Haki za Binadamu ”amesema Mhe. Dkt. Masanja.

Mhe. Dkt. Masanja ametoa wito kwa wajumbe wa kikao hicho kutoa michango yao kwa ukamilifu ambayo pia itasaida wakati THBUB inatoa ushauri kwa serikali.

“Niwaombe kufuatilia kwa umakini wasilisho kutoka kwa wataalam wetu, na kutoa maoni na mapendekezo  yatakayosaidia THBUB kushauri Serikali” amesema Mhe.Dkt Masanja

Awali Katibu Mtendaji THBUB Bw. Patience Ntwina amesema kuwa lengo la Kikao Kazi hicho ni kufanya mapitio ya Sheria mbalimbali zinazohusu Hifadhi za Wanyamapori na Hifadhi za Misitu na kubainisha maeneo yanayohitaji kufanyiwa marekebisho ili kupunguza migogoro iliyopo baina ya wananchi na Mamlaka za Hifadhi katika maeneo ya hifadhi.

 

Bw. Ntwina amesisitiza kuwa pamoja na lengo zuri la kuwepo kwa Sheria za Hifadhi za maeneo husika kwa ajili ya kulinda maeneo hayo, kumekuwepo malalamiko juu ya matukio ya uvunjwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali hususan wakati wa  ukamataji na kuwahoji watuhumiwa na wakati wa kushikilia vielelezo pindi  kesi zinapokuwa zikiendelea Mahakamani; pia kumekuwepo malalamiko ya ukiukwaji wa taratibu za minada ya mifugo inayofanywa katika  hifadhi wakati wa kukazia hukumu za Mahakama pamoja na malalamiko ya urejeshwaji wa mifugo pungufu baada ya kesi kumalizika Mahakamani. Hali hii imesababisha Wananchi kukosa amani na wengine kufilisika na kuleta hasara kwa wafugaji na Taifa kwa ujumla.

"Mengi ya malalamiko hayo yameripotiwa katika kipindi cha takribani miaka nane sasa (8) kwa maana ya kati ya Mwaka 2016 hadi 2023 na katika kipindi hicho yamehusisha Mapori ya akiba ya Wanyamapori na Misitu nchini’’amesema  Bw. Ntiwna.

Kwa upande wake Afisa Sheria Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Cylius Mlekwa amesema kuwa  kikao kazi hiko kina tija kubwa katika kuimarisha na kuboresha mahusiano ya maeneo ya hifadhi na Wananchi waishio pembezoni mwa hifadhi za Taifa.

Bw. Mlekwa ametaja  migogoro hiyo ni  Wafugaji kuingiza mifugo ndani ya hifadhi kwa ajili ya malisho.

“Kupitia kikao hiki ni imani yangu kuwa suluhu itapatikana ya namna bora ya kulinda hifadhi zetu na kuleta tija ya watu” amesema Bw. Mlekwa